Jumanne 24 Novemba 2026 - 21:35
Mapungufu Yaliyosababishwa na Sera za Zamani za Idadi ya Watu Yanapaswa Kufidiwa; Msisitizo Watolewa Kuhusu Kurahisisha Ndoa kwa Vijana

Hawza/ Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia suala la kuongeza idadi ya watu kwa ajili ya mustakabali wa Iran, amesisitiza kuwa: Mapungufu yaliyotokana na baadhi ya sera za zamani kuhusu idadi ya watu yanapaswa kufidiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa Mkutano wa Nne wa Tuzo ya Kitaifa ya Uchangamfu wa Idadi ya Watu, ameitaja sera ya “kuongeza idadi ya watu kwa kuipa familia nafasi ya msingi” kuwa ni sera ya kimkakati na miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za nguvu na maendeleo ya Iran.

Aidha, amesisitiza kwamba: Bila shaka, kila Muirani mwenye uzalendo wa dhati, anayetamani mustakabali wenye matumaini na utukufu kwa nchi hii, ardhi hii na wananchi wake, atakuwa na hamasa na dhamira imara ya kuhakikisha kizazi cha Wairani kinaendelea kuwepo na kuongezeka, kikiwa katika kiwango kinachostahili ustaarabu mpya wa Kiislamu.

Ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambao ulisomwa asubuhi ya leo katika mkutano huo na Bi Marzieh Vahid Dastjerdi, ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Kufanyika Mkutano wa Nne wa Kitaifa wa Uchangamfu wa Idadi ya Watu ni fursa nzuri ya kuzungumzia suala nyeti na muhimu la idadi ya watu. Miongoni mwa nguzo za nguvu, maendeleo na kufikia Iran yenye nguvu zaidi, suala la kuongeza idadi ya watu kwa ajili ya mustakabali wa Iran yetu pendwa, huku yakizingatiwa mahitaji yote yanayohitajika katika nyanja za wingi na ubora, ni miongoni mwa masuala muhimu zaidi.

Suala hili la kimkakati na lenye kuamua hatima ya taifa, ambalo katika miongo ya hivi karibuni lilisisitizwa mara nyingi na Kiongozi Mkuu na Mtukufu wa Mashahidi (Mwenyezi Mungu autukuze zaidi daraja lake takatifu), lina mchango mkubwa katika kuufanya uwezo uliopo kuwa halisi na wenye kuonekana, pamoja na kuunda na kuimarisha fursa mbalimbali za kielimu, kiutamaduni, kiuchumi na kijamii. Vilevile, lina mchango katika kuzuia na kuondoa vitisho pamoja na nia mbaya za maadui.

Inaonekana kwamba, baada ya kipindi kirefu cha kupuuzwa suala hili, hali iliyosababisha hasara kubwa na kutawala katika nyanja za mipango na usimamizi wa mambo ya nchi, sasa, kutokana na baadhi ya hatua zilizochukuliwa, kumepatikana fursa inayowawezesha wananchi na viongozi kulitazama suala hili kwa mtazamo wa kina zaidi.

Katika kuzingatia nyanja mbalimbali zinazohusu idadi ya watu, pamoja na mahitaji na mambo ya lazima yanayohusiana nayo katika maeneo tofauti, wakati mwingine familia na wakati mwingine mtu binafsi hutumika kama kipimo cha kutathmini mambo.

Katika baadhi ya masuala, kama vile makazi na bidhaa pamoja na huduma nyingi, familia ndiyo inayozingatiwa kuwa mtumiaji na mnufaika. Hata hivyo, katika masuala mengine, kama vile chakula, mavazi na mambo yanayohusiana na afya, mtu binafsi ndiye anayezingatiwa kuwa kipimo cha msingi.

Suala la kufikia idadi ya watu inayotakiwa ni miongoni mwa masuala yanayohitaji kuzingatiwa kwa pande zote mbili. Kwa sababu hiyo, kushughulikia aina mbalimbali za miundombinu na nyanja zinazohusiana na kuimarisha msingi wa familia litakuwa ni jambo la kudumu katika juhudi za kurekebisha mwenendo wa mabadiliko ya idadi ya watu nchini. Kadhalika, kushughulikia masuala yanayohusiana na mtu binafsi pia ni jambo la lazima.

Kutilia maanani kwa dhati na kwa mtazamo mpana suala la kurahisisha ndoa katika umri wa ujana; kuhakikisha afya ya mtu binafsi, ambayo yenyewe inategemea mambo mengi mbalimbali; kutoa msaada na kuhimiza uzazi; kueneza utamaduni unaoiweka familia kuwa katika nafasi ya msingi; pamoja na kutambulisha mifano yenye mafanikio katika uwanja huu, kila moja ya mambo hayo ni hatua yenye mchango mkubwa katika kuifanya Iran kuwa na nguvu zaidi.

Vilevile, kuwaeleza wananchi wote, hususan vijana, mambo haya kwa usahihi utakuwa ni msaada mwingine katika kufikia lengo hilo.

Bila shaka, kila Muirani mwenye uzalendo wa dhati, anayetamani mustakabali wenye matumaini na utukufu kwa nchi hii, ardhi hii na wananchi wake, atakuwa na hamasa na dhamira imara ya kuhakikisha kizazi cha Wairani kinaendelea kuwepo na kuongezeka, kikiwa katika kiwango kinachostahili ustaarabu mpya wa Kiislamu.

Nina matumaini makubwa kwamba, kwa kufidia mapungufu yaliyotokana na baadhi ya sera za zamani kuhusu idadi ya watu, pamoja na kufuatilia kwa juhudi na umakini mkubwa sera sahihi na ya kimkakati ya kuongeza idadi ya vijana na kuipa familia nafasi ya msingi katika suala hili, nchi yetu pendwa itaweza kuvuka salama kipindi hiki kigumu na hatua hii nyeti yenye kuamua hatima yake, ambayo kwa sasa inakabiliana nayo.

Aidha, kwa mafanikio yatokanayo na Mwenyezi Mungu na kupitia dua njema pamoja na baraka za Bwana wetu, Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), tunatumai kwamba mazingira na sababu za kushuka kwa baraka za Mwenyezi Mungu kwa Wairani, ambao katika zama hizi wanahesabiwa kuwa wabeba bendera ya haki na uadilifu, zitaendelea kuandaliwa kwa wingi zaidi na kwa namna bora zaidi.

Kwa fadhila na ukarimu Wake.

Sayyid Mujtaba Husayni Khamenei

3 Azar 1405 Hijria Shamsia (24 Novemba 2026).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha